Kwa mara ya kwanza tokea ipate uhuru wake, nchi ya Afrika kusini imeshindwa kupata mshindi wa moja kwa moja kwenye uchaguzi wa serikali kuu na serikali za majimbo. Chama tawala cha ANC kinachoongozwa na rais Ramaphosa kimepoteza viti vingi vya ubunge ambavyo vimenyakuliwa na vyama vya upinzani vya Democratic Aliance, uMkhonto we Sizwe na Economic Freedom Fighters.
Chama tawala cha ANC kilichokuwa na wabunge 230 kabla ya uchaguzi, kimebaki na wabunge 159 kwa mujibu wa matokeo rasmi. Viti hivyo 159 ni sawa ana asilimia 40.18% ya viti vya ubunge, huku chama cha DA kikijizolea asilimia 21.81% ya viti vilivyoshindaniwa katika uchaguzi wa mwaka huu. Chama kipya cha MK kilichoundwa na rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma aliyejitoa ANC kimepata asilimia 14.58% ya viti 400 vilivyoshindaniwa. Chama cha Economic Freedom Fighters kilichopo chini ya mwanaharakati Julius Malema kimeambulia 9.52% ya viti vyote bungeni. Vyama vingine vidogo vilivyoshiriki uchaguzi huo mkuu vimekusanya jumla ya asilimia 13.91%.
Kwa muktadha wa matokeo haya, ni wazi hatma ya muundo wa serikali ya Afrika Kusini haupo mikononi mwa ANC pekee. Ili kupatikana serikali mpya, ANC kitalazimika kuunganisha nguvu na vyama vya upinzani vitakavyoridhia kuwa sehemu ya serikali, ili kuunda serikali itakayokuwa na wingi wa wabunge katika bunge la Afrika Kusini.
Chama cha MK cha Jacob Zuma tayari kilionyesha viashiria vya kutokukubali kushirikiana na ANC chini ya makamu wake wa zamani mh. Ramaphosa.
Katika hatua nyingine, wakati akilihutubia taifa katika mkutano wa tume ya uchaguzi, rais Ramaphosa alitoa rai ya mshikamano na utulivu kwa raia wan nchi hiyo, huku akiwapongeza kwa ukomavu wa kidemokrasia waliouonyesha katika kipindi kizima cha harakati za uchaguzi.
Rais Ramaphosa pia alizipongeza jumuiya za kimataifa zilizotuma wawakilishi wa uangalizi katika uchaguzi huo huku akitamka kuwa matokeo yaliyotangazwa na muitikio wa mapokeo yake kutoka kwa wananchi wa Afrika Kusini ulikuwa kiashiria cha ushindi kwa watu wote wa Afrika Kusini.
Akitoa ujumbe kwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo, mwenyekiti wa chama tawala na rais wa Afrika Kusini mh. Cyrill Ramaphosa aliwaasa kuweka mbele maslahi ya taifa lao na kuepuka ubinafsi. Akitoa msimamo wa chama chake, aliweka bayana kuwa watakauwa tayari kuunganisha nguvu na chama chochote kitakachokuwa tayari kuwatumikia watu wa Afrika Kusuni.