Mabingwa wa ligi kuu nchini Tanzania, yanga afrika, wameibwaga klabu ya azam ya jijini Dar es salaam katika fainali ya kombe la fa iliyofanyika jana Zanzibar. Fainali hiyo iliyokuwa ya kukata na shoka huku kila timu ikionyesha ubora wa hali ya juu iliamuliwa kwa matuta ya penati baada ya muda wa kawaida wa dakika tisini na zile za nyongeza kutamatika bila nyavu za timu yeyote kutikisika.
Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wengi, azam ilianza kipindi cha kwanza kwa kishindo kwa kumiliki sehemu kubwa ya mchezo katika kipindi cha kwanza. Licha ya umiliki wa muda mrefu, hakukuwa na hatari yeyote iliyolifikia goli la yanga waliokuwa na tahadhari kubwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa yanga kuupoka umiliki wa mchezo kutoka azam na kutengeneza mashambulizi kadhaa ya hatari yaliyozuiliwa na kipa wa azam aliyekuwa katika kiwango bora kwenye mchezo wa jana.
Baada ya dakika tisini kutamatika, muda wa dakika thelathini za nyongeza ulitumika kwa tahadhari kubwa kwa timu zote mbili ambazo zilionekana kupunguza kasi ya kushambuliana.
Muda wa kujua mbivu na mbichi uliwadia wakati wa matuta ya penati ambayo kwa upande wa yanga azizi ki (alikosa), Guede (alikosa), Pacome (alipata), Yao (alipata), Bakari Nondo (alipata), Aucho (alipata), Musonda (alipata), Ibrahim (alikosa), Mkude (alipata).
Penati za azam zilipigwa na Mutasingwa (alipata), Sidibe (alipata), Fuentes (alikosa), Sillah (alikosa), Kipre (alipata), Manyama (alipata), Feisal (alipata), Mwaikenda (alikosa) na Iddi Nado (alikosa). Kwa maana hii yanga waliibuka washindi kwa penati 6 kwa 5 za azam.
Mechi hiyo jana ilikuwa inahitimisha msimu wa mashindano kwa ngazi ya vilabu nchini Tanzania ambao umekuwa wa ushindani mkubwa.