Nadharia za uongozi na falsafa za kiutawala duniani kote zinaangazia zaidi kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili raia, lakini zaidi kufungua fursa mbalimbali za nyanja tofauti tofauti kwa watu. Moja kati ya nguzo muhimu za utawala wa kiinchi, duniani kote ni pamoja na mashirikiano na nchi nyingine na washirika mbalimbali wasiobeba sifa za kiinchi kama mashirika ya kimaendeleo na mengine mengi ya jinsi hiyo.
Ukamilifu wa historia ya Tanganyika na baadae Tanzania una mizizi yake katika mahusiano ya kidiplomasia yaliyoasisiwa na baba wa taifa la Tanzania mwl. Julius K. Nyerere na waliokuwa wawakilishi wa dola ya kifalme ya Uingereza.
Marais wa awamu zote sita (6), kila mmoja kulingana na zama na changamoto uuongozi wake uliopitia waliwekeza katika kuiweka Tanzania katika ramani ya kidiplomasia ili kuendana na kasi ya ukuaji wa maendeleo duniani lakini pia kuunganisha nguvu katika kuzikabili changamoto za pamoja kwa umoja.
Moja kati ya sanaa mpya tunazozishuhudia katika awamu hii ya sita (6) chini ya Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni ufanyaji na uendeshaji wa diplomasia ya uchumi kama nyenzo ya kuchochea mageuzi ya kiuchumi. Katika zama ambazo dunia kwa ujumla wake inakabiliwa na changamoto ngumu kuliko nyakati nyingine zozote zile, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uthubutu, utayari na umahiri wa kukabiliana na changamoto zinazousumbua ulimwengu.
Rais Samia amedhihirisha ubunifu wake kupitia diplomasia ya utalii, kwa kuingia makubaliano na kurekodi filamu mahiri ya Tanzania The Royal Tour. Kupitia filamu hii, sekta ya utalii nchini iliyokuwa imedorora kutokana na janga la uviko 19 iliamka na kushuhudia ongezeko la idadi ya watalii tofauti na ilivyokuwa awali.
Diplomasia ya mikutano imekuwa njia nyingine inayotumika na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuifungua nchi yet una kuiweka kwenye ramani za vituo bora zaidi barani Afrika vya kufanyia mikutano mikubwa yenye tija za kidunia. Tanzania ya rais Samia Suluhu Hassan inahesabika kama sehemu salama zaidi barani Afrika kwasasa, ambacho ni kigezo muhimu zaidi katika kuvutia mikutano mingi mikubwa.
Utayari wa rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuyapa kipaumbele mahitaji ya kidunia nao umekuwa kivutio kikubwa kwa mataifa mengine na mashirika ya kimataifa. Kupitia moyo huu wa kipekee wa rais Dkt. Samia, mataifa na mashirika mbalimbali duniani yamevutika kuwekeza rasilimali, hasa fedha kwenye miradi mingi ya kimaendeleo inayotekelezwa na serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwenye zama hizi ambazo zimegubikwa na mdororo wa kiuchumi duniani kote na vita za kiuchumi pamoja na za misituni, rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejikita zaidi katika diplomasia chanya ya kufungua milango ya uwekezaji, kwa kuboresha mazingira na kuanzisha vivutio vya kipekee vitakavyoitofautisha Tanzania na nchi nyingine.
Ushahidi wa kimatokeo wa kazi za kidiplomasia zinazofanywa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unadhihirisha kuibeba pia jumuiya ya Afrika mashariki ambayo ina mashirikiano na mahusiano ya kimkakati na Tanzania. Kupitia dira ya maendeleo ya taifa, ni wazi uthabiti wa serikali inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu una dhamira ya dhati ya kuipaisha Tanzania kiuchumi. Kwa kutambua kuwa Tanzania sio kisiwa kinachojitosheleza peke yake na kujitegemea, rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaweka historia nyingine ya kipekee kwa kuipeleka Tanzania juu zaidi ya pale ambapo isingefika bila kujengewa mkakati madhubuti wa dplomasia ya uchumi inaoufuata sasa.